Mwanamke wa Kiislamu wa Brazil anasema nini kuhusu hijabu?

“Camila Celestino”, bibi wa Kiislamu wa Brazil, ni mmoja wa wale ambao, katikati ya giza la ujinga na kutofahamu, wakawa mfano wa aya «اللَّهُ وَلِیُّ الَّذینَ آمَنوا یُخرِجُهُم مِنَ الظُّلُماتِ إِلَی النّورِ»   “Mwenyezi Mungu ni

… na Waumini wanaotutoa gizani na kutupeleka kwenye nuru” na kupata hijabu ya fatimiyya katika Maisha yake.  Katika kuendelea, tutasoma mahojiano na bibi huyu wa Brazil na kupata kujua mtazamo wa bibi huyo wa hali ya juu kuhusiana na Uislamu na hijabu.

 Bi. Camila, kabla ya Uislamu ulikuwa na dini gani?

Nililelewa katika familia ya Kikristo.  Familia yangu ilikuwa ya kidini sana na kuanzia umri wa miaka 8, mama yangu alinipeleka kanisani kusomea mambo ya dini, lakini hilo lilinifanya niwe na maswali na mashaka juu ya dini ya Kikristo, kama vile kwa nini tunajadili Utatu wa Mungu katika dini ya Kikristo, kwa nini Mimi namwita Yesu mwana wa Mungu, au kwa nini tunaimba “Ee Mariamu Mama wa Mungu” katika mojawapo ya maombi muhimu ya Wakristo?  Hali ya kua katika Biblia yenyewe imeandikwa kwamba Mungu aliumba kila kitu, basi Mungu anawezaje kuwa na mama??!

Au Mkristo Mkatoliki anatakiwa kukiri dhambi yake kwa padri ili aombewe msamaha kwa Mungu ili atuambie tufanye nini ili Mungu atusamehe, lakini sikuweza kukubali kwa nini tumwendee mtu ambaye na yeye ni mtenda dhambi .Tukiri ili Mungu atusamehe!  Nilikuwa na maswali mengi akilini mwangu ambayo sikuweza kupata majibu.  Nilienda kanisani kujifunza masomo ya dini hadi nilipokuwa na umri wa miaka 12-13, lakini baada ya muda, kutokana na kutopata majibu ya maswali haya, nilihisi kwamba Ukristo si dini kamili, na ndiyo sababu niliiacha dini hii.  Kwa upande mwingine, niliamini kwamba hakuna Mungu  kwa muda fulani kutokana na matatizo fulani kama vile ugonjwa wa mama yangu na matatizo ya kiuchumi.

 Ni nini kilikufanya kuingia kwenye dini ya Uislamu?

Siku moja wakati niko shuleni, mwalimu alipokuwa akiuliza kuhusu dini za watoto, mtoto fulani alisema, “Dini yangu ni Ubudha.”  Nilijua kwamba Wabudha hawamwamini Mungu, na ndiyo sababu nilitaka kuzungumza naye zaidi, na ndiyo sababu nilihudhuria mikutano ya mtu huyu wa Kibudha kwa takriban mwaka mmoja na nusu, lakini wazazi wangu walipinga vikali.  Huko Brazili, mtu hubadili dini kwa urahisi, lakini ili kubadili  baadhi ya dini, mtu lazima awe na umri wa zaidi ya miaka kumi na minane na lazima  apate ruhusa ya wazazi, lakini wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 16 na wazazi wangu hawakuridhika kamwe kwamba niingie kwenye dini ya kibudha;  Ndiyo maana niliacha dini ya Buddha na sikwenda dini nyingine yoyote, hadi nilipokua na umri wa miaka 18 nilianza kufanya kazi katika duka la kamera za kupiga picha, ambalo mmiliki wake alikuwa ni  MLebanoni na Mwislamu.  Bila shaka nililazimika kufanya kazi huko kutokana na matatizo ya kifedha, kwa sababu sikuwapenda Waislamu na dini ya Kiislamu hata kidogo, lakini niliona tabia ya Muislamu huyu inavutia sana;  Kwa mfano alikuwa hatoi mkono kwa wanawake na alikuwa akiweka mkono wake kwenye kifua chake kama ishara ya heshima na kuwaambia wanawake kuwa thamani yako ni kubwa sana na siruhusiwi kukugusa;  Au kwa mfano, aliwaheshimu binti zake zaidi ya wanawe wa kiume.  Tabia ya mwanaume huyu kwa wanawake ilifanya mawazo yangu hasi kuhusu Uislamu na Waislamu kubadilika kidogo kidogo.

Siku moja alinipa kitabu kiitwacho “Mtume na Familia yake”.  Nilipokifungua kitabu, Surah Ikhlas iliandikwa kwa Kireno, na katika Sura hii, nilipata jibu la maswali yangu yote, na hili lilinifanya niwe na shauku ya kutaka kujua zaidi kuhusu Uislamu, lakini hata hivyo, sikuwa na nia ya kuwa  Muislamu.  Baada ya kukisoma kitabu, nilifika kwenye kisa cha Imamu Husein (AS) na Karbala, na hapo ndipo nilipokata tamaa na sikuweza kukabiliana na dini hii na kutoikubali.  Karibu miezi sita ilipita tangu siku niliposoma kitabu hiki hadi siku niliposema Shahadataini, kwa sababu kujifunza sheria za Uislamu na kusoma surah kwa Kiarabu kulichukua muda, lakini nilisilimu nikiwa na umri wa miaka 19 na baada ya kupata njia ya kuingia katika Uislamu.

 Je, uliikabili vipi familia yako katika swala la kubadili dini yako?

Wazazi walishangaa kidogo, kwa sababu kuna mtazamo hasi kuhusu Uislamu nchini Brazili;  Kwa vile Waislamu wanatajwa kuwa ni magaidi na Uislamu ni dini yenye ukatili, ndio maana wazazi wangu hawakupenda niwe Mwislamu, lakini nilipozungumza nao kuhusu imani ya Kiislamu walikubali na mama yangu aliniunga mkono sana nilipochagua kuvaa hijabu.

Je, baada ya kusilimu kwako, familia yako haikubadili dini?

Hapana!  Familia yangu bado ni ya Kikristo.  Katika miaka hii michache, niliweza kuwabadilisha baadhi ya watu kuwa Waislamu na wengine kutoka Sunni kua shia, lakini kamwe silazimishi familia yangu, kwa sababu ninaamini kwamba ikiwa mtu anataka kufanya kitu, moyo wake unapaswa kukubali;  Bila shaka mimi natekeleza wajibu wangu kuhusiana na dini ya Kiislamu, lakini sio mikononi mwangu kusilimu kwa mtu , ni mkono wa Mwenyezi Mungu, na siwezi kuwalazimisha wengine kuukubali Uislamu, kama tunavyosoma katika Qur’an, “Laa Ikrah Fi Al-Din”.

 Baada ya kuwa Muislamu, ulikumbana na changamoto gani katika jamii?

Wale ambao walikuwa na elimu au angalau wenye elimu ndogo ya dini ya kweli ya Uislamu walikuwa wananiheshimu sana na wakati mwingine hata wale ambao hawakuwa na elimu juu ya dini ya Kiislamu waliniheshimu, lakini kulikuwa na kundi ambalo lilikuwa na mtazamo hasi juu ya Uislamu na wao waliwasumbua Waislamu sana.  Nakumbuka kwamba mara moja katika treni ya chini ya ardhi, mtu mmoja alinishambulia kwa sababu ya hijabu yangu, na wakati mwingine, katikati ya jiji, mtu fulani alinirushia takataka, lakini sikuwahi kuwalaani watu hawa, kwa sababu ninahisi kwamba watu hawa kwa bahati mbaya wameathiriwa na Habari za Televisheni, redio na mitandao ya kijamii zimeeneza uongo kuhusu Uislamu na Waislamu na hawajawahi kuchunguza iwapo habari hizi za uongo kuhusu Uislamu ni za kweli au laa.

Tafadhali tuelezee wakati bado hukua na hijabu; mavazi yako yalikuaje? 

Nilipokuwa Mkristo, mavazi yangu yalikuwa ya kawaida, lakini nilipokuwa mkubwa, nilijaribu kuvaa nguo ndefu na pana, kwa sababu sikujisikia amani hata kidogo, na labda kama sio hisia hii nisingeweza Kwenda   kwenye hijabu na stara hata kidogo, na kwa kweli ninapokua na hijabu kamili kwenye jamii najihisi salama na amani sana.

 Ulijisikiaje kabla na baada ya kuvaa hijabu?

Kabla sijawa Mwislamu, nilijaribu kuvaa nguo ndefu na zisizobana kwa sababu ya macho yenye kuudhi ya wengine, na bado nyakati nyingine nilitaniwa na wengine.  Siku zote nilitaka kufanya kitu ili kujilinda, na kwa vile nimekuwa Muislamu na kujisitiri, ninahisi usalama na uhuru, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kunitazama jinsi anavyotaka.  Nilipoona hijabu kwa karibu, ilinivutia sana kwa kuwa inafunika sehemu zote za mwili, na nilihisi kwamba thamani yangu imeongezeka kwa sitara;  Ndio maana nasisitiza kuvaa hijabu katika nchi yangu ya Brazil.  Nilichagua hijabu kwa moyo wangu na hakuna mtu aliyenilazimisha, kwa sababu nilihisi kuwa dini yangu ingekamilika zaidi kwa kuvaa hijabu.

 Ikiwa unataka kulinganisha hijabu na kitu, unalinganisha na nini?

Katika moja ya vita, Jibril alimteremkia Mtume (SAW) na kumletea zawadi ya dua ya [jaushan kabiir] kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili imlinde.  Dua ya Jushan Kabir ina maana ya nguo ya vita ambayo inaweza kumlinda mtu kutokana na balaa lolote.  Nami Ninaifananisha hijabu, na haswa sitara ya jilbab, na jushan kabiir kwa mwanamke ambayo inaweza kumlinda dhidi ya macho ya matamanio.  Pia mimi naamini hijabu ni bendera ya dini ya kiislamu,kwa sababu ukimuona muislamu yuko katika nchi ya kikristo au nchi isiyo ya kiislamu hutajua kuwa ni muislamu au la, lakini ukimuona mwanamke mwenye stara, utajua kuwa yeye ni Muislamu kwa sababu ya hijabu yake.

 Kwa maoni yako, hijabu ya Kiislamu ina ufanisi gani katika kupunguza uhalifu na ubakaji katika jamii?

Hijabu ina ufanisi mkubwa sana katika kupunguza uhalifu.  Kwa bahati mbaya, baadhi ya wapinzani wa sheria ya hijabu sio tu kwamba wanaona kutovaa hijabu kuwa hakuna ufanisi katika kupunguza uhalifu, lakini pia wanadai kuwa kutokuwepo kwa hijabu katika jamii za Magharibi kunasababisha kuhalalisha ngono, lakini mimi sikubaliani na hili hata kidogo. kwa sababu kama ripoti zinavyoonyesha, takwimu za ubakaji katika nchi za nje kama vile Brazil, Amerika, Uingereza na nchi nyinginezo zisizo za Kiislamu ni nyingi zaidi ya nchi za Kiislamu kama Iran. Kiukweli  Hijabu ni nzuri sana katika kupunguza uhalifu na ubakaji, hasa kwa mtazamo wa kitamaduni, na kwa kuvaa hijabu,  tunaweza kupata jamii yenye usalama zaidi.

Wewe Kama mwanamke ambaye umeishi katika jamii isiyo ya Kiislamu na umeonja maisha katika jamii ya Kiislamu, una ushauri gani kwa wale wanaopenda utamaduni wa Magharibi?

Mimi mwenyewe nilikuwa mtu ambaye nilipenda Amerika, Uingereza na nchi za nje na nilikuwa na ndoto ya kuishi Amerika, New York na California.  Hata Marekani ilipoingia Iraq, nilikuwa nikiipendelea Marekani na fikra yangu ilikuwa kwamba Marekani inapaswa kuwaua Wairaqi, lakini nilipoifahamu dini ya Kiislamu, nilitambua kwamba hatufaidiki chochote katika maisha haya isipokuwa matendo yetu. Na hakuna bora kuliko  kuwa na dini kamilifu ambayo itatuongoza kwenye furaha duniani na akhera.

Wakati mwingine binadamu huwa mkaidi na hata kukabiliana na dini, nchi na utamaduni wake.  Tunapaswa kuweka kando ukaidi huu na ikiwa tuna maswali yoyote, tusipinge tu, bali tujaribu kutafuta majibu ya maswali na mashaka yetu.  Jambo lingine ni kwamba, kwa bahati mbaya, mitazamo ambayo watu wanayo kutoka nje ya nchi sio sahihi kabisa.  Tunachokiona kwenye filamu za kigeni ni tofauti sana na ukweli.  Katika filamu, wanajaribu kuonyesha mambo mazuri tu, wakati kila nchi, ikiwa ni pamoja na Amerika, ina mambo mazuri na mabaya;  Kwa hiyo, hatupaswi kudanganywa na mwonekano wa nje wa udanganyifu wa Magharibi.  Watu wanaonizunguka mara nyingi huniambia, “Kwa nini hukubaki Brazil na umekuja Iran, Brazil ni bora zaidi kuliko Iran” mimi nawajibu kwamba: wewe unaesema Brazil ni bora kuliko Irani uliwahi kufika huko? “Mpaka tupate uzoefu wa kuishi katika nchi Fulani kwa karibu, ndio tutaweza kuona ubora wa nchi hio na sivyenginevyo. Mimi  Kama mtu ambaye nimepitia maisha katika nchi isiyo ya Kiislamu, nasema kwamba ninajivunia kuishi Iran.